Shirika la Madini la Taifa la STAMICO linatarajiwa kuwa ifikapo mwaka 2024/2025 kuzalisha kwa wingi mkaa mbadala unaotokana na Makaa ya Mawe, Kuimarisha uchimbaji mkubwa wa makaa ya Mawe pamoja Kuongeza uwekezaji wake kwa lengo la kuboresha shirika hilo kwa manufaa makubwa ya Taifa.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika Hilo Dk.Venance Mwasse wakati akieleza utekelezaji wa shughuli za shirika kwa wahariri na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam ikiwa ni mwendelezo na utaratibu wa msajili wa hazina Nehemiah Mchechu kuzitaka Taasisi na mashirika ya Umma kukutana na wanahabari kuzungumzia utekelezaji wake.
Amesema shirika hilo pia lina mikakati ya kuendeleza wachimbaji wadogo na kuhakikisha wanashiriki katika uvunaji wa rasilimali kupitia uchimbaji pamoja na kuwasaidia kupata vifaa, mitaji na kuwaunganisha na wadau husika na hatimae kujikwamua kiuchumi.
Akieleza mafanikio yaliyopatikana katika shirika hilo amesema ni kuongezeka kwa Mapato ya ndani kutoka Shilingi Bilioni 1.3 kwa Mwaka 2018/19 Hadi Shilingi Bilioni 61.1 kufikia mwaka 2022/23 pamoja na Kutekeleza mkakati wa Kuwasaidia wachimbaji wadogo na kuwapa mafunzo na vifaa.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile mbali na kulipongeza shirika hilo kwa uzalishaji mkubwa ameshauri shirika kuweka mipango Mikakati na kipaumbele kwenye maslahi ya wafanyakazi kwa kuwaongezea mishahara pale shirika linapokua ili kuwapa ari mpya ya utendaji.