BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limesema litashirikiana na halmashauri pamoja na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kutoa elimu  kwa wenye mabasi na magari ya mizigo katika utunzaji wa mazingira kutokana na uwepo wa tabia kusimamia porini kwa lengo la kujisaidia maarufu kama kuchimba dawa. 

NEMC itatoa elimu kwa muda wa mwezi mmoja, Kuanzia wiki ijayo baada ya hapo basi litakalokamatwa, litapigwa faini ya Tsh. Milioni tano.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa NEMC Dkt. Samuel Gwamaka amesema moja ya jambo ambalo limekuwa likifanyika mara kwa mara kama mazoea ni mabasi ya abiria, malori na magari yanayofanya safari ndefu kuwa na kawaida ya kusimama porini kwa lengo la kujisaidia (kuchimba dawa).


Amesema tabia hiyo imechangia kuchafua mazingira na kuwa kero kwenye jamii, kwani hali hiyo imekuwa ikifanyika hata katika vyanzo vya maji na hivyo wakati wa mvua uchafu unasambaa na kuharibu mazingira.