Na Beatrice Kaiza 


Kamishna wa Bima Tanzania Dkt. Baghayo Saqware  amesema Sekta ya Bima imekua kwa wastani wa asilimia 12.8% kwa mwaka ambapo kwa kipindi cha miaka mitano mauzo ghafi ya bima yameongezeka kutoka Tsh. Bilioni 691.9 mwaka 2018 hadi kufikia  takribani Trilion 1.2 mwaka 2022.


Aidha Mchango wa Sekta ya Bima kwenye pato la Taifa unazidi kuongezeka kutoka asilimia 0.56% kwa mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 1.68% kwa mwaka




Akizungumza na Waandishi wa habari Dkt. Saqware amesema Mamlaka ya usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imeendelea kuongeza gawio Serikalini ambapo kwa kipindi cha Julai 2022 hadi Juni 2023 Mamlaka imeweza kulipa gawio kwa Serikali la jumla ya Tsh. Bilioni 2.9.


Aidha amesema Sekta ya bima imechangia kwenye ajira kwa vijana ambapo hadi Septemba 2022 imetoa ajira za kudumu kwa Watanzania 4, 173.


Pia Dkt. Saqware amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2022/2023 Mamlaka imepata mafanikio kadhaa ikiwa ni pamoja na Uanzishaji wa Konsotia ya Bima ya Kilimo, Uanzishaji wa Konsotia ya Bima ya Mafuta na Gesi Tanzania , lakini pia kurekebisha sheria ya Bima na Kanuni zake.


"Mantiki ya kuanzisha konsotia ni kuhakikisha miradi yote ya gesi na mafuta inabakiza sio chini ya asilimia 45 ada zitokanazo na gesi na mafuta; kufuatia kutokuwa na uwezo wa soko la ndani, vihatarishi vya nishati, vilielekezwa nje ya Nchi kwa asilimia 100. Jambo ambalo sio na lisilo na tija kwenye uchumi wa nchi, amesema Dkt. Saqware.


Aidha, kuanzishwa kwa miradi mikubwa ya nishati kama vile bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) ni fursa kwenye sekta ya bima kujipanga kwa ajili ya kuongeza tija, uchumi na ajira nchini."


Kutokana na hivyo Dkt. Saqware amesema Mamlaka inaendelea na mkakati wake wa utoaji wa elimu kwa umma kwa kushirikisha wadau wote kwenye sekta, Lengo ni kufikia asilimia 80% ya watanzania wote wenye umri wa miaka zaidi ya kumi na nane (18) ifikapo mwaka 2030.


“Lengo la mkakati ni utoaji elimu ya bima na uhamasishaji wa  Serikali, Idara, Taasisi za Umma ili ziweze kuzingatia Sheria ya Bima Sura 394, kif.133 (1) hadi (3), kif.140  na Sheria ya Umma Na. 7 ya Mwaka 2011, kif. 4 (2) (b)


"Hadi mwezi Julai 2023, Mamlaka imezitembelea Wizara za Kilimo; Wizara ya Nishati na Wizara ya Uchukuzi na Ujenzi na TAMISEMI."


"Mkakati huu ni endelevu na utazifikia Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Umma." Alisema


Kuhusu utekelezaji wa miradi, Mamlaka, kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2019/2020 hadi 2021/2022, imetekeleza miradi miwili ya Mifumo ya TEHAMA (TIRAMIS na TIRA-ORS), mifumo hiyo yote imejengwa na watumishi wa umma.



Kwa upande wa kulinda haki za mteja wa Bima, Mamlaka imeendelea kuzisimamia kampuni za bima kuhakikisha zinalipa madai na fidia stahiki kwa wakati na kwa haki ambapo hadi sasa ulipaji wa madai na fidia stahiki kwa wateja wa bima yamefikia asilimia 95 hivyo kupungua kwa malalamiko. 


Hata hivyo asilimia 5 ya madai na fidia yana changamoto ambazo TIRA inafuatilia na kutoa suluhisho.



"Kwa mfano, ulipaji wa madai ya bima za kawaida uliongezeka kwa asilimia 10.1 kutoka shilingi bilioni 301.9 mwaka 2021 hadi shilingi bilioni 332.09 mwaka 2022. 

Malipo ya madai na mafao ya bima za maisha yaliongezeka kwa asilimia 29.3 kutoka bilioni 95.7 mwaka 2021 hadi bilioni 123.71 mwaka 2022.

Jumla ya kiasi  cha madai kilicholipwa mwaka 2022 ni shilingi bilioni 455.80 hivyo, kupunguza umaskini kwa wanufaika na kufanya biashara kuwa endelevu." Alisema Dkt. Saqware 


Aidha, Mamlaka inaendelea na uendeshaji wa  mikutano ya kupokea na kusikiliza malalamiko ya bima kwa wananchi ambapo hivi karibuni Mamlaka imefanikiwa kuandaa mikutano mitano katika kanda zote za Mamlaka.


"Katika mwaka huu wa fedha wa 2023/24 Mamlaka imeanzisha mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi ili kuifanyia marekebisho sheria ya Bima na Kanuni zake. Mchakato huu umeanzishwa kufuatia maboresho ya mifumo ya usimamizi wa Bima na maendeleo ya soko la bima nchini."