Na Beatrice Kaiza
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) pamoja na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC) kwa pamoja wanalaani vikali kukamatwa kwa Wakili Boniface Mwabukusi pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu, Wilbroad Slaa na Mpaluka Said Nyagalt.
Akizungumza leo na waandishi wa habari Dar es Salaam 15 August, 2023 Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Wakili Anna Henga, amesema kuwa Mawakili wa watuhumiwa hao wametueleza kwamba tuhuma zinazowakabili ni kosa la uhaini ambapo wamehojiwa kwa nyakati tofauti katika vituo vya Polisi.
“Hata hivyo taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa Agosti 12, 2023 ilieleza kwamba Boniface Mwabukusi na Mpaluka Nyagali walikamatwa majira ya saa nane na nusu usiku wa tarehe 12/08/2023 maeneo ya Mikumi Morogoro. Taarifa hiyo inaeleza kuwa ni watuhumiwa waliandaa na kutoa maneno ya uchochezi. Wakili wa Dr. Slaa naye alitueleza kwamba Dr.
Slaa alikamatwa Agosti 13, 2023 na kupelekwa kituo cha Polisi Mbweni, baadae alienda kupekuliwa nyumbani kwake na hatimae alipelekwa kituo cha Polisi Oysterbay. Akiwa kituo cha Polisi Oysterbay, Dr. Slaa alihojiwa kwa tuhuma za uchochezi lakini baadae tuhuma zikabadilishwa na kuhojiwa tena kwa tuhuma za uhaini, kama ilivyofanyika kwa Wakili Mwabukusi na Nyagali
Kutokana na taarifa ya Jeshi la Polisi pamoja na taarifa kutoka kwa mawakili wa watuhumiwa, ni dhahiri kwamba watuhumiwa walikamatwa kwa tuhuma za uchochezi lakini fuhuma za uhaini walipewa kwenye vituo vya Polisi, hii ni kinyume na kanuni za kimataifa za upelelezi wa makosa va jinai
Hivi karibuni wakili Mwabukusi pamoja na wanaharakati wengine wa haki za binadamu akiwemo Wakili Peter Madeleka ambaye amefutiwa makubaliano ya hati ya kukiri kosa, wamekuwa wakishiriki katika mijadala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongea na vyombo vya habari kuhusu mkataba wa uwekezaji wa bandari ulioingiwa kati ya Serikali ya Jamhuri va Muungano wa Tanzania na Emirati ya Dubai huku wakieleza mapungufu kadhaa ya mkataba huo ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri kwa Serikali,” amesema Henga
Aliongezea kuwa “Sisi kama mashirika ya Haki za Binadamu tunaamini kwamba Watetezi wa Haki za Binadamu wana haki ya kutoa maoni kuhusu jambo lolote katika nchi yetu ikiwemo kuhusu maboresho ya mkataba wa bandari na hawastahili kupata vitisho au kukamatwa kwasababu ya Intumia uhuru wao uliopo kikatiba na unaolindwa na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia,” amesema Henga.
Aidha ikumbukwe kuwa Rais Samia wakati alipokuwa anapokea Taarifa ya Tume ya kuangalia jinsi ya kuboresha taasisi za haki jinai nchini alisisitiza kwamba wale wanaokosoa kwa hoja wajumuishwe kwenye tume ya Mipango na sio kuwatishia au kuwakamata. Hatua inayoendelea sasa, sio tu inaenda kinyume na nia ya Mheshimiwa Rais ya kuboresha mfumo wa haki jinai na kujenga Demokrasia chini kupitia Falsafa ya "R' nne, bali vanaenda kinyume na Katiba ya Tanzania na Mikataba ya Kimataifa ambayo inalinda Haki za Binadamu.



