Bank ya Taifa ya Biashara NBC hii leo August 31 2023 wametangaza rasmi mashirikiano kati yao na Mamlaka ya Usimamizi Wa Bima Nchini (TIRA) katika uendeshaji wa akaunti ya dhamana (Trust Account) kwa kampuni za bima Nchini.
Hatua hiyo inakuja mara baada ya TIRA Kuanzisha akaunti ya dhamana ambayo ina masharti na Bank ya NBC imetimiza masharti hayo yenye lengo la kuimarisha sekta ya bima nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyoambatana na semina maalumu kwa wadau wa sekta ya bima nchini Jijini Dar es Salaam Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania TIRA Dkt. Baghayo Saqware amesema akaunti hiyo ilianzishwa mahususi ili kuhakikisha wanaepusha changamoto ya kampuni za bima kutumia fedha za dhamana ya mitaji bila ruhusa ya Kamishna wa Bima
Dkt Saqware amewahakikishia watanzania kwamba kampuni za bima Nchini wanazozisimamia zina ukwasi wakutosha na zinaweza kulipa madai ya Bima kwa wakati ambayo yamekwishaiva.
“Hapo awali kulikuwa na changamoto ndogo ambapo kampuni za bima zilikuwa na kiwango cha fedha katika Benki ya Tanzania (BoT) lakini kiwango hicho huwekwa kwenye hati fungani na zinapoiva zinarudi katika akaunti ya kampuni ya bima hivyo tukawa tunapata changamoto ya baadhi ya kampuni hizi kutumia fedha hizo bila ruhusa ya Kamishna wa Bima “Amesema Dkt.Saqware.
Ameongeza kuwa wanategemea kuwapa wateja wao huduma bora kupitia mfumo wa kieletroniki ambapo Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania itakuwa inafuatilia mwenendo huo.
“Sisi NBC ni benki ambayo imekuwepo kwa miongo mitano hivyo tunayo furaha kutoa mafunzo haya kwa wadau wa bima pia Benki ya NBC imejipanga vyema katika kutoa ushauri wa uwekezaji kupitia Idara yetu ya Hazina na Masoko ya Mitaji hivyo nitoe wito kwa makampuni ya bima nchini kuzingatia taratibu zilizowekwa” Amesema Bw. Sabi.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa TIRA Bw. Abubakar Ndwata amesema chimbuko la Akaunti hiyo ya Dhamana ya Bima ni Kanuni ya Bima ya mwaka 2009 inayozitaka Kampuni za Bima kuweka Amana za Usalama angalau 50% ya kiwango cha chini cha mtaji halisi wa kampuni husika ya bima.
Ndwata amesema TIRA kwa kushirikiana na Chama cha Makampuni ya Bima Tanzania (ATI), wamekubaliana kuandaa Mwongozo wa Uwekezaji na Usimamizi wa Ukwasi ambao pia ulielekeza uanzishwaji wa Akaunti ya Dhamana ya Akiba kupitia benki za biashara ili kuondokana na tatizo la changamoto ya kimtaji au kushindwa kulipa fidia za madai ya wateja wake.



