Kufuatia tukio la vifo vya mapacha wawili njiti waliodaiwa kuuawa huku wakiondolewa baadhi ya viungo vyao mara baada ya kuzaliwa katika hospitali ya Kaliua mkoani Tabora, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema watumishi waliohusika wamesimamishwa kazi.
Waziri Ummy amesema uchunguzi uliofanyika umebaini kuwa jambo hilo ni la kweli na kumuagiza RMO wa Tabora kusimamia vyema weledi, maadili na miiko ya watumishi wa afya.
“Tumelifuatilia suala hili, kuna ukweli. Uongozi wa (W) Kaliua umeshaanza kuchukua hatua. Baadhi ya Watumishi wa Afya waliomuhudumia mama huyu wameshasimamishwa kazi. Nakemea vikali kitendo hiki. Ninamuagiza RMO Tabora kusimamia vyema weledi,maadili na miiko ya watumishi wa afya,” amesema.
Kupitia mtandao wa Facebook, anayedaiwa kuwa baba mzazi wa mapacha hao, Kisaka Mtoisenga amesema watoto walizaliwa salama licha ya kuwa njiti, na kwa kuwa kituo hicho hakina uwezo wa kuhudumia watoto njiti, kituo kiliwapa rufaa kwenda hospitali teule ya Wilaya na kuwashauri watafute usafiri binafsi kwani kituo hakina gari la wagonjwa.

