WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kazi kubwa imefanyika katika kipindi cha awamu hii ya uongozi kwa kutekeleza mikakati na sera zinazolenga kuondoa ubaguzi na kukuza usawa wa kijinsia.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumapili, Desemba 3, 2023) wakati akizungumza na maelfu ya wananchi waliohudhuria kilele cha maadhimisho ya tatu ya kumbukumbu ya kumuenzi mwanasiasa mkongwe, Bibi Titi Mohammed yaliyofanyika kwenye viwanja vya Ujamaa, Ikwiriri, wilayani Rufiji, mkoani Pwani.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema: “Pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali, asasi za kiraia na jumuiya ya kimataifa, bado kuna changamoto nyingi katika kufikia usawa wa kijinsia. Ukweli huo unatoa msukumo muhimu wa kuendeleza na kuimarisha juhudi zetu katika kushughulikia masuala ya usawa wa kijinsia,” amesema.
Akitaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali ya awamu ya sita, Waziri Mkuu amesema ya kwanza ni kuongeza idadi ya wanawake katika nafasi za maamuzi ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa fursa mbalimbali za uongozi kwa wanawake na kuimarisha uwiano katika teuzi anazozifanya kitendo ambacho kimeongeza idadi ya wanawake katika uongozi.
“Maamuzi haya ya Mheshimiwa Rais ni mfano wa utambuzi wa nafasi ya mwanamke na fursa kwa wanawake na kuthamini umuhimu wa kuwa na uwakilishi wa kutosha wa wanawake katika ngazi mbalimbali za uongozi.”
Amezitaja hatua nyingine kuwa ni kufanya maboresho kwenye mfumo wa elimu ili kuongeza fursa zaidi, kutekeleza mipango mahsusi ya kuhakikisha jamii ya Tanzaia inakuwa na afya bora na inashiriki kikamilifu shughuli za ujenzi wa Taifa na pia kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia mikopo na mafunzo kwa wajasiriamali wa kike ili waweze kujikwamua kiuchumi.
"Serikali pia inatekeleza afua na mikakati mbalimbali ya kuondoa mila na desturi potofu ambazo zimekuwa zikizuia maendeleo ya wanawake. Naamini kuwa tamasha hili litazidi kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika jamii yetu. Tushikamane sote na tuendelee kujenga Tanzania yenye usawa na haki kwa wote," amesisitiza.
Akiweka msingi wa kuendelea kumuenzi mkongwe huyo, Waziri Mkuu amesema: “Namna bora ya kuenzi mchango mkubwa wa Bibi Titi ni kwa kuiga uchapakazi wake. Hivyo basi kila mmoja katika nafasi yake afanye kazi kwa bidii, uzalendo na ujasiri.”
“Maadhimisho haya ni ya kihistoria na yanatukumbusha kuwa uhuru tulionao ni kazi iliyofanywa na wazalendo, mashujaa wa nchi waliokuwa tayari kufa kwa ajili ya nchi yao. Aidha, yanaikumbusha jamii ya Watanzania kuwa mwanamke ana nafasi kubwa katika harakati mbalimbali za kitaifa,”amesema.
Amewataka wananchi wote washirikiane na Serikali kupinga kwa nguvu zote ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto. “Kila mmoja wetu aone kuwa ni wajibu wake kuwalinda watoto wa kike na wa kiume. Dunia ya sasa imeharibika kutokana na mmomonyoko wa maadili, hivyo basi sote tupaze sauti kukemea matendo yote maovu. Tumieni madawati ya jinsia pamoja na vyombo vyote vilivyopo katika mifumo ya jamii zetu kuwaripoti wahusika wa vitendo vya ukatili.”
Mapema, Waziri wa Nchi (OR - TAMISEMI), Mohammed Mchengerwa alisema maadhimisho hayo yalihusisha shughuli mbalimbali ikiwemo upandaji miti, kugawa vitanda kwenye shule ya sekondari ya Bibi Titi na kuweka jiwe la msingi kwenye daraja la Bibi Titi lililopo kwenye barabara ya kwenda Mohoro.
Akiwa kwenye mabanda ya maonesho kwenye maadhimisho hayo, Waziri Mkuu alielezwa kwamba shule mpya za msingi 302 zimeshajengwa na ziko tayari kupokea wanafunzi 1,093,000 wanaotarajiwa kuanza kidato cha kwanza mwakani na kwamba wote wataanza kwa awamu moja.
Akitoa taarifa hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano (OR-TAMISEMI), Bi. Ntee Hosea alisema: “Katika kutekeleza mikakati ya kuboresha ufundishaji na ujifunzaji shuleni, ulioanza kutekelezwa Januari 2023 hadi sasa, idadi ya wanafunzi wanaomudu stadi za KKK darasa la kwanza na la pili imeongezeka kutoka asilimia 35 hadi asilimia 94.”
Alisema wanafunzi wenye kumudu lugha ya Kiingereza kwa kiwango cha kujitambulisha darasa la tatu kwa shule za Serikali imeongeza kutoka asilimia 45 hadi asilimia 80 na wanafunzi wanaomudu stadi nne za kutumia lugha ya Kiingereza kidato cha kwanza imeongezeka kutoka asilimia 38 hadi asilimia 87.