Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 20,2023, Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa umoja huo, Martin Mbwana akiwa ameambatana na viongozi wengine wa Jumuiya hiyo amesema kuanzisha kampeni hiyo ni kumuunga mkono kazi na juhudi za Rais Samia.
“Kwanza ni kwa ule uhuru aliotupatia wafanyabiashara wa Kariakoo, pili kwa huduma za kijamii ambazo anaendelea kuzifanya katika nchi yetu, hususani Dar es Salaam yetu, tatu ni uwekezaji ambao ameanza kuufanya kwenye Bandari yetu ya Dar es Salaam. Hivyo tumekubaliana kuwa na kampeni ya Tuvushe Mama 2025, tukiamini kwamba tuko na Mama, hatutamuacha Mama, kushikamana nae Mama hadi mwaka 2025 tutakapovuka salama katika uchaguzi mkuu,” alisema mwenyekiti huyo.
Aidha Mbwana alisema kuwa hivi karibuni kulikuwa na matatizo ya hapa na pale na namna ya ufanyaji biashara kwao ulivyokuwa na sintofahamu za hapa na pale, lakini kupitia uongozi wa Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Awamu ya Sita leo mfanyabiashara wa Kitanzania, wazawa wanafanya kwa uhuru.
“Leo Kariakoo ina amani, mfanyabiashara wa Kariakoo anafanya kwa uhuru na wamerudi kwa kasi kufanyabiashara, wageni wanakuja na nchi imefunguka. Kwa hiyo tunamshukuru sana mama, tunaishukuru Serikali yake kwa ujumla kwa sapoti kubwa waliyotupa ambapo leo hii tuna amani kubwa na Mamlaka ta Mapato Tanzania (TRA), tunafanyabiashara zetu vizuri na tunalipa kodi vizuri,” alisema Mbwana.


