SHIRIKA la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) wameikabidhi shirika la Reli Tanzania(TRC) makasha matano(5)yenye majokofu ya kuhifadhia na kusafirisha bidhaa ya matunda na mbogamboga ili kuikuza kilimo cha Bustani, Makasha(Makontena) hayo yana thamani ya Dola za kimarekani laki 337 sawa na shilingi za kitanzania milion 840,Tukio la makabidhiano limefanyika leo Jumatatu Septemba 11,2023 katika karakana ya TRC, Chang'ombe Jijini Dar es salaam.
Tanzania ni miongoni mwa wazalishaji 20 wakubwa duniani wa mazao ya bustani yanayovunwa moja kwa moja kutoka shambani, sekta ya kilimo cha bustani ni sekta inayokua kwa kasi zaidi ndani ya sekta ya kilimo ya taifa, ambayo inaongozwa na wakulima wadogo wadogo, na inawakilisha asilimia kubwa na muhimu ya pato la taifa linatokana na kilimo.
Hata hivyo, pamoja na maendeleo makubwa yaliyopatikana na umuhimu wa kilimo cha bustani kwa uchumi, kiasi kikubwa cha mazao ya bustani(kinachokadiriwa kuwa kati ya asilimia 30 hadi 40) hupotea katika mnyororo wa thamani, na sababu kubwa ni ukosefu wa hifadhi ya baridi.
Mnyororo wa thamani ya chakula kuanzia kwenye uzalishaji hadi kwa utumiaji, ni safari ndefu, Bidhaa zinazoharibika kwa haraka, kama vile za kilimo cha bustani, zinahitajika kupozwa ili kuzuia kuoza na kuharibika, na mradi wa pamoja kati ya TRC na WFP kuhusu maendeleo ya mnyororo baridi wa masoko ya kilimo, Kati ya Dodoma/Morogoro /Dar es salaam unategemea kushughulikia hili haswa.
WFP imekuwa ikiwaunganisha wakulima wadogo wadogo na masoko tangu mwaka 2009.Mradi huu utatoa usafiri wa uhakika, salama, na gharama nafuu, kwa ajili ya mazao ya kilimo cha Bustani kuanzia kwenye uzalishaji hadi kwenye masoko, kwa ajili ya kuwawezesha wazalishaji wadogo wadogo na wakusanyaji wa mazao kufika kwenye masoko. mbalimbali. Huduma hii itawasaidia pia wauzaji wa rejareja, wasindikaji wa chakula, na wauzaji wa bidhaaa nje ya nchi na mkazo maalum utawekwa kwa wanawake na vijana.
Akiongea na vyombo vya Habari mgeni rasmi wa Halfa hiyo Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa Makame Mnyaa Mbarawa amesema "Napenda kuwashukuru TRC na WFP kwa kunipa heshima ya kuwa mgeni rasmi katika halfa hii ya makabidhiano ya makasha ya ubaridi ambapo mashirika haya mawili yameingia katika makubaliano ya kutoa huduma ya usafiri wa bidhaa za mbogamboga na matunda katika mikoa ya Dodoma, Morogoro na Dar es salaam "
"Ili kuhakikisha wakulima wanaondokana na changamoto za mazao kuharibika na gharama kubwa za usafirishaji kwa kukosa miundombinu rafiki ya kusafirisha na kuhifadhi mazao ya mbogamboga na matunda, TRC ikishirikiana na WFP imekuja na mradi wa kuwasidia wakulima kusafirisha mazao kwa urahisi zaidi kwa kutumia mabehewa yenye makasha yanayohifadhi ubaridi kwa nyuzi joti Arobaini"alisema Waziri Prof. Makame Mbarawa



