Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema inathamini mchango wa Asasi za Kiraia katika kutekeleza mipango na sera mbalimbali za maendeleo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amebainisha hayo katika uzinduzi wa Warsha ya Baraza la Umoja wa Afrika la Uchumi, Kijamii, na Utamaduni la Umoja wa Afrika (ECOSSOC) Jijini Dar es Salaam
Dkt. Shelukindo amesema kuwa Serikali ya Tanzania chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inathamini mchango wa Asasi za Kiraia kwa sababu Serikali imekuwa ikipanga Mipango na Sera mbalimbali lakini kwenye utekezaji Asasi za Kiraia zinahusika kwa kiasi kikubwa. Hivyo kwenye utekelezaji lazima kuwe na asasi za kirai zenye ubora.
“Serikali imekuwa ikipanga Mipango na Sera mbalimbali lakini kwenye utekezaji Asasi za Kiraia zinahusika kwa kiasi kikubwa. Hivyo kwenye utekelezaji wa sera na mipango hiyo inahitaji kuwa na asasi za kirai zenye ubora,” alisema Balozi Shelukindo
“Nimeona mada mbalimbali za leo katika Warsha hii ya leo zinazungumzia mambo mengi kama vile misingi ya kidemokrasia, haki za binadamu na utawala bora na vitu vya msingi katika kukuza uchumi wa nchi yetu ambapo vitu vyote vinakwenda sambamba,” aliongeza Dkt. Shelukindo.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania Nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Afrika (AU), Balozi Innocent Shiyo amesema Warsha hiyo ni muhimu ambapo mwaka 2002, uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) uliibadilishwa na kugeuzwa kuwa Umoja wa Afrika. Lengo la hayo ilikuwa ni kuongeza ushiriki wa wananchi kwenye shughuli za Umoja wa Afrika. Ili kufikia azma hiyo, mwaka 2004, Umoja wa Afrika ulipitisha Mkataba wa kuanzisha Baraza la Uchumi, Kijamii na Kitamaduni (ECOSOCC).
“Baraza la Uchumi, Kijamii na Kitamaduni linatoa fursa kwa asasi za kiraia zilizopo Barani Afrika kushiriki kwenye shughuli za Umoja wa Afrika kwa kutoa ushauri kwenye Vyombo vya Kisera vya Umoja wa Afrika na kuwaelimisha pia wananchi kuhusu mipango na mikakati mbalimbali ya Umoja wa Afrika ili kurahisha utekelezaji wake,” alisema Balozi Shiyo.
Balozi Shiyo aliongeza kuwa utendaji kazi wa Baraza la Baraza la Uchumi, Kijamii na Kitamaduni la umoja wa Afrika unafanyika kwenye ngazi ya Kanda, ambapo kila nchi inawakilishwa kwenye Kamati Tendaji (Permanent General Assembly). Sambamba na hilo, kila nchi ina jukumu la kuanzisha Jukwaa la Kitaifa (ECOSOCC National Chapters) lengo likiwa ni kuhamasisha asasi nyingi zaidi za kiraia kwenye nchi kushiriki kwenye masuala ya Umoja wa Afrika.
“Lengo la warsha ni kuzihamasisha na kuongeza uelewa na uwezo wa Asasi za Kiraia za Tanzania kushiriki kwenye shughuli za Umoja wa Afrika. Pamoja na Mambo mengine, Warsha hii itasaidia kuongeza ushiriki na uelewa wa Asasi za Kiraia na Watanzania kwa ujumla kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na Umoja wa Afrika,” aliongeza Balozi Shiyo.
Naye Mkuu wa Mkuu wa Sekretarieti ya ECOSOCC, Bw. William carew amesema kuwa ECOSOCC itasaidia kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya Umoja wa Afrika (AU) na Asasi za Kiraia nchini Tanzania. Hivyo kutoa fursa ya jukwaa la ushirikishwaji katika kutafuta Afrika bora.
“lengo letu kama ECOSOCC ni kusaidia kuimarisha ushirikiano kati ya Umoja wa Afrika (AU) na Asasi za Kiraia Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla,” alisema Br. Carew.
Tanzania ni miongoni mwa nchi ya tano za awali kuanzisha majukwaa ya kitaifa ya Ecosocc ili kuwa karibu na asasi za kiraia kwa lengo la kuhamasisha maendeleo nchini pamoja na kufikia malengo ya Ajenda ya 2063 inayohusu masuala mbalimbali ikiwemo elimu, afya, demokrasia na mengineyo. Mbali na Tanzania, nchi nyingine ni pamoja na Mauritius, Siare Leone, Zambia na Misri.