Na Beatrice Kaiza
WANANCHI na wadau mbalimbali wa maendeleo wametakiwa kujitokeza kwa wingi ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa ya kutokomeza maambukizi ya virusi vya ukimwi hadi kufikia mwaka 2030.
Rai hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Afisa Mtendaji mkuu wa Baraza la Taifa la watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Tanzania (NACOPHA) Deogratius Peter ambapo amebainisha kuwa baraza hilo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu wamedhamiria kufikia maambukizi sifuri ya virusi vya ukimwi ambapo kwa sasa takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya watu wanaojua kuwa wanaishi na virusi vya ukimwi imefikia asilimia 96, watu waliopima na wanaoendelea na matubabu imefikia asilimia 98 huku ambao tayari virusi vyao vimefubazwa ikiwa imefikia asilimia 97.
Aidha amebainisha kuwa baraza hilo kwa kutambua umuhimu wa mapambano dhidi ya maambukizi ya ukimwi wameandaa tamasha lenye lengo ya kukusanya rasilimali fedha zitakazowezesha afua mbalimbali za mapambano hayo linalotarajiwa kufanyika mnamo Agosti 11 mwaka huu ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila.
Kwa upande wake mwenyekiti wa vijana wanaoishi na virusi vya ukimwi Pudeliana Mbwiliza amesisitiza kuwa wadau hawana budi kuungana kwa pamoja ili kuhakikisha nguvu kazi ya taifa inalindwa dhidi ya maambukizi mapya ya ukimwi ili kuongeza ushiriki wao katika shughuli mbalimbali za maendeleo huku akiwaasa waathirika wanaojificha kujitokeza kwa jamii na hivyo kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya virusi hivyo.








