WAZIRI Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameipongeza Benki ya NMB kwa kutenga fedha zaidi ya sh. bilioni 40 kwa ajili ya kuwawezesha vijana na wanawake kwenye Mpango wa Kuwaandaa Vijana na Wanawake kwa Kesho iliyo Bora (BBT).

Mpango huo ni kupitia kilimo, uvuvi na ufugaji, pamoja na kushuka kwa riba ya mikopo ya sekta hizo za kimkakati hadi kufikia asilimia tisa.


Majaliwa ametoa pongezi hizo alipotembelea Banda la NMB kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Nane Nane yanayofanyika katika Viwanja vya Mwakangale jijini Mbeya, ambapo ameelezwa kuwa katika kipindi cha miaka miwili, benki hiyo imetenga sh. bilioni 40, zikiwemo sh. bilioni 20 za mikopo ya kuunga juhudi za BBT na sh. bilioni 20 zingine ni kwa ajili ya mikopo ya ujenzi wa maghala ya kukabiliana na upotevu na uharibifu wa mazao baada ya mavuno.

Hata hivyo Majaliwa alimuuliza Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ambaye alikuwa ameongozana nae kwenye maonesho hayo,ili kujiridhisha kama ni kweli Benki ya NMB imepunguza riba kwenye mikopo ya kilimo hadi kufikia asilimia tisa.

“Mheshimiwa Waziri wa Kilimo (Hussein Bashe), ni kweli kwamba riba ya mikopo ya kilimo, uvuvi na ufugaji
imeshuka kiuhalisia na kufikia asilimia tisa! Hongereni sana kwa kushusha riba kutoka double digit (yaani tarakimu mbili) hadi kufikia single digit (tarakimu moja). Ni matumaini yangu itashuka zaidi hadi asilimia nane au saba (7)” ameuliza na kupongeza Majaliwa.