Na Beatrice Kaiza 


Chama cha watu wenye ualbino Tanzania (TAS) kwa pamoja na kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wamelaani vikali kitendo kilichofanywa siku ya Simba Day August 6, 2023 na kumtumia mtu mwenye Ualbino mithili ya mtu aliyekua katika hali ya nusu utupu na aliyevaa nepi ya mkojo jukwaani mbele ya kadamnasi ya maelfu pale uwanja wa taifa.

Akizungumza leo Dar es Salaam 9 August, 2021 Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Wakili Anna Henga, amesema wanatoa wito kwa jamii ikiwemo watu wenye albino nchini kutochukulia vitendo vya aina hii kwa wepesi, na badala yake kuvikemea vikali kwa maana watu wenye albino ni binadamu wenye haki ya kutodhalilishwa na kuheshimiwa utu wao. 


“Tunautaka ongozi  wa Simba uombe radhi kwa watu wenye ualbino na umma wa watanzania kwa vitendo hivi vya kutweza utu  wa watu wenye albino  na pia tunatoa wito kwa jamii ikiwemo watu wenye albino wenyewe kutochukulia vitendo vya aina hii kwa wepesi, na badala yake kuvikemea vikali,” amesema  Henga.

Aliongezea kuwa kuwaomba Serikali na TFF wasimamie jambo hili.



Kwa upande wa Mwenyekiti Taifa Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) Godson Mollel  amesema kuwa Tukio hili linafuatia tukio jingine lililofanywa na timu hii mwaka jana tarehe 8/8/2022 siku ya Simba day ambapo kulitokea kitendo cha kutumia jeneza, msalaba na kumnasibu mtu mwenye ualbino kama msukule. 


“Vitendo hivi vinatweza utu wa watu wenye ualbino nchini na vinapelekea kuwepo kwa mijadala mingi katika jamii ikiwemo mitandaoni inayoonesha dhihaka kwa watu wenye albino kinyume na haki za binadamu,” amesema Mollel 



Ameongezea kuwa Ikumbukwe kwamba, kwa miaka mingi sasa kumekua na jitihada kubwa za utetezi wa watu wenye albino chini kutokana na historia ya madhila yaliyopelekea watu wenye albino kupoteza maisha, pamoja na idadi kubwa ya wahanga wa vitendo vya ukatili na unyanyapaa. Wakati huohuo jamii ikiwa na kawaida ya kuwachukulia watu wenye albino kiujumla kwa taswira walizozoea kuziona hususan kwa njia ya mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.


“Katika jamii nyingi watu wenye ualbino Wamekuwa wakihusishwa na mila na tamaduni mbaya zinazotweza utu wao. Hivyo, kuendelea kwa viyendo hivi ni kudidimiza juhudi za serikali, mashirika watetezi na wadau binafsi 2a kuelimisha jamii kuhusu albino,” amesema Mollel.