Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE) kimefanya Mkutano wa Utambulisho wa Bodi mpya ya ATE uliotanguliwa na Mkutano wa 63 wa Bodi hiyo ambapo Mgeni Rasmi alikuwa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Lazaro Ndalichako (MB).
Katika hotuba yake, Waziri Ndalichako pamoja na mambo mengine amesisitiza kuwa suala la kufanya kazi katika UTATU ni la kisheria ambapo masuala yote yanayohusiana na Kazi na Ajira yanajadiliwa na wadau hao yaani ATE, TUCTA na Serikali na kuwasihi Bodi Mpya ya ATE kuwa ni muhimu kuendeleza mahusiano mazuri miongoni mwao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa ATE, Bw. Oscar Mgaya ameahidi wataendeleza mahusiano na wadau wa UTATU ili kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini kwa ustawi wa Sekta ya Kazi na Ajira kwa kufuata misingi ya Katiba ya Chama lakini pia Sheria, Kanuni na Taratibu.
Hapo awali Afisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Bi. Suzanne Ndomba-Doran alifanya wasilisho kuhusu Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na namna kinavyofanya kazi huku akigusia muundo wake, majukumu yake na namna kinavyoshirikiana na wadau wake.
Mkutano huo umehudhuriwa pia na Mwakilishi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Bw. Amani Msuya ambaye amewapongeza ATE kwa kuandaa Mkutano huu na kuwaomba kuendeleza ushirikiano katika kutatua changamoto mbalimbali kwenye maeneo ya Kazi.
