Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC), limesema lipo kwenye mchakato wa kutengeneza kituo mama cha gesi Dar es salaam ili kurahisisha upatikanaji wa gesi nchi nzima kwa lengo la kutoa huduma ya gesi majumbani na kwenye magari
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Mohamed Makame wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari mapema leo Julai 20 jijini Dar es Salaam ambapo amesema Mradi unaotekelezwa ni kujenga kituo mama cha usambazaji wa gesi iliyoshindiliwa maeneo ya Mlimani City.
Aidha amesema kituo hicho kitakuwa kinashindilia gesi ili iwekwe kwenye malori ambayo yatakuwa yakisambaza gesi katika vituo vitakavyojengwa.
Mkurugenzi huyo ameongeza kwa kusema wametoa pia fursa kwa kampuni binafsi kujenga vituo vitakavyotoa huduma ya gesi ili kufikia lengo la kusambaza huduma hiyo maeneo mbalimbali Tanzania.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa utafutaji na uendelezaji gesi asilia Keneth Mutaonga amesema shirika hilo lipo katika hatua za mwisho kuelekea kuanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa gesi wenye thamani ya dola billion 42 ambao utaongeza gesi , pato la taifa na kutengeza ajira.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri wa vyombo vya habari Deogratus Balile amesema miradi hiyo inafaida kubwa kwa taifa na kuwataka waandishi wa habari kuisemea miradi hiyo pamoja na kutoa uelewa kwa wananchi ili kuondoa baadhi ya upotoshaji ambao umekuwa ukisambazwa kwenye jamii juu ya masuala mbalimbali.
" Kwanza wafahamu kwamba yale wanayoyatenda hayana nafasi ya kufahamika na jamii bila vyombo vya habari, hakuna kiongozi atakayepata nafasi ya kutembelea nyumba kwa nyumba, Mkoa kwa Mkoa ama wilaya kwa Wilaya au kijiji kwa kijiji ili kufikisha taarifa za utendaji wao ndio maana wanapaswa kushirikiana na sisi" amesema Balile
Shirika hilo la Maendeleo ya petrol nchini limefanya Mkutano na Jukwaa la wahariri wa vyombo vya habari leo Julai 20 ,2023 ikiwa ni agizo la Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu ambaye amezitaka taasisi na mashiriki kuwa na mikutano ya mara kwa mara na Jukwaa la wahariri wa vyombo vya habari ili kufahamu mengi juu ya taasisi hizo.


