Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Joyce Ndalichako amekabidhi Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) magari 13 na vifaa vya ukaguzi vyenye thamani ya zaidi ya bilioni 2 ambavyo vimetolewa na  Serikali ili kuboresha utendaji wa Taasisi hiyo.

Vifaa na magari  vyenye thamani ya jumla ya bilioni 4 vimekabidhiwa leo (Juni 30, 2023) katika hafla maalum iliyofanyika katika Ofisi za OSHA zilizopo Kinondoni jijini Dar es Salaam. 



  Hafla hiyo ilienda sambamba na ufunguzi wa mafunzo kwa watumishi wapya 18 ambao wameajiriwa ikiwa ni mkakati wa kuendelea kuboresha utendaji wa OSHA.



Akizungumza katika tukio hilo, Waziri Ndalichako amesema  vifaa na magari na vimenunuliwa ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais, Samia Suluhu Hassan, aliyoitoa katika maadhimisho ya Mei Mosi mwaka huu yaliyofanyika Kitaifa Mkoani Morogoro ambapo alieleza kuwa  Serikali yake imepanga kuiongezea hadhi Taasisi ya OSHA.


“Haya yote yanafanyika leo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wetu mpendwa, Samia Suluhu Hassan aliyoitoa katika hotuba yake akiwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) 2023 yaliyofanyika Kitaifa Mkoani Morogoro. 


Rais aliahidi kununua magari 13 na kuajiri watumishi wapya 18 ili kuiongezea Taasisi ya OSHA uwezo zaidi wa kutekeleza majukumu yake,” ameeleza Waziri Ndalichako na kuongeza:



“Kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) napenda kutoa pongezi na shukrani zangu za dhati kwa Rais wetu Mama Samia kwa kutambua umuhimu wa Taasisi ya OSHA hapa nchini na kuamua kwa dhati kuipandisha hadhi na kuipa uwezo zaidi wa kutekeleza jukumu lake la msingi la kulinda nguvukazi ya Taifa hili pamoja na mitaji ya wawekezaji kwa kuwezesha upatikanaji wa vyombo hivi muhimu vya usafiri, vifaa vya kaguzi pamoja na kuongeza idadi ya watumishi.”


Kwa mujibu wa Waziri mwenye Dhamana ya Masuala ya Kazi, uwezeshaji huo wa  Serikali kwa OSHA utaongeza kasi na hamasa kwa taasisi hiyo katika shughuli zake.