Jumla ya wanafunzi 593 wamenufaika na mfuko wa SAMIA Scholarship wenye shilingi 2,754,370,430.00 kwa ajili ya wenye ufaulu wa juu katika masomo ya sayansi katika kidato cha sita ambao wanaendelea kusoma masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati au Afya na Sayansi Shirikishi kwenye ngazi ya shahada.


Akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2023/24 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. ADOLF MKENDA amesema serikali imetoa jumla ya Shilingi 652,763,079,647.00 kupitia Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.


“Shilingi 652,176,491,647.00 zimetolewa kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma ndani ya nchi ambapo 586,588,000.00 kwa wale wanaosoma nje ya nchi ikiwa na jumla ya wanufaika 202,877. Mwaka wa kwanza wapo 72,973 na wanaoendelea na masomo 129,904,” amesema Prof. Mkenda


Ili kuwezesha utekelezaji wa malengo kwa mwaka wa fedha 2023/24, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (Fungu 46) inaomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 1,675,753,327,000.00.