Msanii staa wa Bongofleva Alikiba na Mchezaji staa Mbwana Samatta wanatarajia kukusanya fedha kupitia mechi ya hisani inayolenga kusaidia matibabu ya Watoto njiti Kibiti Mkoani Pwani na Kigoma kupitia Samakiba Foundation kwa kushirikiana na Doris Mollel Foundation ambayo kwa miaka saba imekuwa ikijishughilisha na kutoa misaada mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia Watoto njiti.
Akiongea katika kuzindua kampeni hiyo waliyoipa jina la ‘Nifuate na Upendo wa Zambarau 2023', AliKiba amesema hii ni awamu ya sita ya mechi hizo za hisani ambapo kwa mwaka huu wanaungana na Doris Mollel Foundation.
Kiba amesema “Taasisi ya Doris Mollel imekuwa ikisaidia Serikali kutoa huduma kwa Watoto njiti na kusaidia utoaji wa vifaa vya afya vinavyotumika kuokoa maisha ya Watoto njiti hivyo tumeona tuungane nao katika kuwasaidia Watoto wetu hawa”
“Kutakuwa na Bonanza mbili za mitaani, zilizopangwa kufanyika June 10 na 11, 2023 maeneo ya Kariakoo na Mbagala huku mechi ya hisani ikiwa imepangwa kufanyika June 17,2023 Chamazi Azam Complex”
Kwa upande wake Doris Mollel amesema katika kampeni hiyo wamechagua Kigoma na Kibiti kwakuwa ndio maeneo yenye idadi kubwa ya kuzaliwa kwa Watoto hao njiti ukilinganisha na Mikoa mingine ambapo kupitia Samata na Kiba watawezesha kuwafikia Watu wengi zaidi katika utoaji elimu na pia fedha zitakazopatikana zitatumika kununua vifaa na kuanzisha utoaji wa huduma katika vituo vya afya badala ya kufata huduma hiyo Hospitali za Rufaa.



